Friday, December 13, 2019

Mashindano ya Watoa Huduma Bora na Salama ya Usafirishaji Abiria

 

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

 

sumatraLogo.png - 52.49 KB

 

TAARIFA KWA UMMA

MASHINDANO YA WATOA HUDUMA BORA NA SALAMA YA USAFIRISHAJI ABIRIA


Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) imeanzisha mashindano ya watoahuduma Bora na Salama yatakayofanyika kwa kuwashindanisha watoa huduma ya usafiri wa masafa marefu na hatimaye kutoa tuzo kwa mtoa huduma atakayeongoza kwa kuendesha shughuli za usafirishaji abiria kwa ubora na usalama zaidi. Mashindano hayo yatafanyika kila mwaka na tuzo maalum kutolewa katika tukio litakalofanyika katika maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani inayoadhimishwa mwezi Septemba wa kila mwaka.

Pamoja na mambo mengine, madhumuni ya mashindano hayo ni kuhimiza udhibiti wa ndani baina ya watoa huduma ili kuimarisha ubora na usalama wa huduma ya usafiri wa abiria hapa nchini. Pia tuzo hii inatarajiwa kuhamasisha uwepo wa utamaduni wa usalama kwa wadau wa sekta ya usafiri. Aidha mashindano hayo yatatoa fursa ya kuonesha utendaji wa mfano (best practice) na uzoefu wa watoahuduma katika kuimarisha usalama katika sekta ya usafiri.

Mashindano yatawahusisha watoahuduma za usafiri wa mabasi ya masafa marefu. Mashindano yataanza kwa kushirikisha watoahuduma wakubwa na wa kati ambapo watoahuduma wengine watahusishwa katika kipindi kijacho cha mashindano.

 

Vigezo vitakavyotumika katika mashindano hayo ni kama ifuatavyo:

 1. Idadi ya matukio ya ajali yaliyotokea katika kipindi cha mashindano ambacho ni mwaka mmoja
 2. Utunzaji wa kumbukumbu za matukio ya ajali katika kipindi cha mashindano

 3. Uwepo wa mpango mahsusi na mfumo wa matengenezo ya mabasi

 4. Uwepo wa ajira rasmi za wafanyakazi. Mikataba ya ajira kwa wafanyakazi

 5. Uwepo wa dawati/mfumo maalum la huduma kwa wateja na kushughulikia malalamiko ya abiria

 6. Mpango wa kutunza mazingira ikiwemo vyombo vya kukusanya taka katika mabasi

 7. Ukusanyaji wa maoni ya abiria kuhusu ubora wa huduma. Hii ni pamoja na kuwepo dodoso kwa ajili ya abiria kutoa maoni yao kuhusu huduma zinazotolewa na basi husika

 8. Utekelezaji wa masharti ya leseni ya usafirishaji abiria. Idadi ya hati ya kupatikana na makosa (Notifications) mbalimbali katika utoaji huduma ya usafiri kutoka SUMATRA na Jeshi la Polisi

 9. Uwepo wa Mpango wa Ubora na Usalama

 10. Umbali uliotumika katika kutoa huduma katika kipindi cha mashindano. Vitabu vya batli (Log Books) na uwepo wa mfumo wa ufuatiliaji wa mwenendo wa mabasi utatumika katika kubaini iwapo basi au kampuni husika imekuwa ikitoa huduma ya usafirishaji katika kipindi cha mashindano

 11. Uwepo wa madereva wawili kwa mabasi ya safari ndefu zaidi ya kilometa 700

 12. Kuwepo kwa wataalam wa usafirishaji katika kampuni husika kama inavyoelekezwa na kanuni za udhibiti wa usafirishaji abiria.

Ili kuleta uwazi na uwajibikaji katika kuendesha mashindano hayo, Kamati maalum inayojumuisha wataalam kutoka taasisi zinazohusika na masuala ya usalama wa usafiri hapa nchini imeundwa na kupewa jukumu la kumpata mtoa huduma atakayestahili kupata tuzo hii.

Katika kutekeleza na kufanikisha zoezi hili, watoa huduma wanaelekezwa kuvipitia vigezo vyote vilivyotajwa na kuandaa nyaraka zinazohusiana na vigezo hivyo ili kuweza kuwa washindani wa tuzo hiyo. Ni vema ikaeleweka kuwa mashindano hayo yatatoa fursa kwa mtoa huduma atakayeshinda kujitangaza zaidi kibiashara na hivyo kuendelea kushamiri katika sekta ya usafiri wa abiria katika eneo analotoa huduma na kwingineko.

Ni matarajio ya Mamlaka kuwa wadau, hususan wamiliki wa mabasi ya masafa marefu watatoa ushirikiano unaohitajika ili kufanikisha zoezi hili muhimu katika kuimarisha ubora na usalama wa usafirishaji abiria nchini.

Usafiri Bora na Salama Unawezekana!

Imetolewa na:

 

Gilliard W. Ngewe

Mkurugenzi Mkuu

Januari, 2017